IRELAND YARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI WA ARDHI PACSO

NAIBU Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mags Gaynor, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa umiliki wa rasilimali ardhi kwa wanawake, uliokuwa ukitekelezwa na Mwemvuli wa asasi za kirais Pemba ‘PACSO’ na kumalizika hivi karibuni.

Naibu Balozi huyo alisema, kutokana na majibu ya wanufaika wa mradi huo alivyozungumza nao, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, na hasa kwa kuwafikia walengwa.

Alisema mradi huo ulilenga kuwafikia wanawake ili kuwajengea uwelewa, juu ya umilikiwa wa rasilimali ikiwemo ardhi, jambo ambalo sasa, limewanufaisha hasa kwa kuwepo wanufaika waliopata haki zao.

Naibu Balozi huyo aliyasema hayo ofisi za PACSO Chake chake Pemba, kwenye kikao cha tathimi kilichojumuisha wanufaika wa mradi wa uongozi wa PACSO.

Alieleza kuwa, kwa vile wapo wanawake kisiwani Pemba walionufaika moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na kurithi, kununua ardhi na kulalamikia ucheleweshaji urithi ni hatua kubwa.

“Serikali ya Ireland, imeridhishwa mno na mradi huu uliokuwa ukiendeshwa na ‘PACSO’ na tutangalia uwezekano wa kuendeleza kuhusiasna na elimu kwa jamii,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Naibu huyo Balozi wa Ireland Mags Gaynor, alisisitiza haja kwa wanufaika hao kuwafikishia wenzao elimu ya umuhimu wa umiliki rasilimali.

Alisema kuwapa mradi huo PACSO rasilimali fedha hazikupotea, kutokana na kuwanufaisha walengwa, waliokuwasudiwa ndani ya jamii husika.

Mmoja wa wanufaika hao Fatma Khamis Juma wa Wawi, alisema awali hakuwa akiona umuhimu wa umiliki wa rasilimali, ingawa baada ya mafunzo, sasa ameamka.

“Hata urithi sasa tumesharithi, maana niliwaambia kaka zangu kuwa sasa turithi, na tumesharithi baada ya kuwaelimisha ingawa walikuwa wazito,’’alieleza.

Mratibu wa miradi kutoka PACSO, Mohamed Najim Omar, alisema licha ya mradi huo kuwa wa miezi miwili, lakini umefikia lengo lao.

“Pamoja na kwamba mradi ulikuwa wa miezi mwili, lakini wanawake kwa asilimia 60 na wanaume asilimia 40, walifikiwa na kunufaika kwa kupata elimu,’’alieleza.

Nae Salama Mtondoo kutoka Wete, alisema licha ya kuwa na kesi yake mahakamani ya kutapeliwa na kiongozi wa serikali ardhi yake, lakini mafunzo hayo yamempa hamasa zaidi.

“Mafunzo ya umiliki wa ardhi, na hasa siku ile ya kuzitambua sheria za ardhi, kwangu yamenipa uwelewa zaidi, wa kuendelea na kesi yangu,’’alieleza.

Sheha wa shehia Vitongoji wilaya ya Chake chake, Ayoub Suleiman, alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Febuari alipokea malalamiko 40 ya wanawake juu ya ardhi.

“Baada ya kupata mafunzo ya umiliki wa rasilimali hasa ardhi, sasa hata malalamiko katika shehia yangu yameongezeka kutoka 25 ya mwaka 2021, hadi kufikia 40 kwa kipindi cha miezi mwili kwa mwaka huu,”alisema.

 

Afisa Mipango wilaya ya Chake chake Kassim Ali Omar, alisema wamepokea maombi 20 kwa mwaka huu, ya wanawake wakiomba kununua na kuuza ardhi zao.

Katibu mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, alisema mradi huo wanatarajia unawezaa mwengine kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata.

Katika utekelezaji wa mradi huo, awali kulifanyika uzinduzi wa mradi, kongamano, mafunzo ya siku nne ya umiliki ardhi pamoja na kuzifahamu sheria za usimamizi ardhi.