RC kusini Pemba atoa neno kwa NGOs

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema uwepo wa asasi nyingi za kiraia nchini, iwe ni chachu ya kuchapuza maendeleo ya nchi na hayo yatajitokeza iwapo zitafanya kazi kwa bidii.

Mkuu huyo wa mkoa, aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa mkutano wa kuwasilisha rasimu ya mswada wa sheria ya Jumuiya zisizo za serikali nambari 6 ya mwaka 1995, mkutano ulioandaliwa na mwenvuli wa asasi za kiraia Pemba, ‘PACSO’ ambao umefanyika kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake.

Alisema, serikali inathamini kwa kiasi kikubwa, mchango wa NGOs, hivyo uwepo wake kwa wingi nchini, iwe sababu ya kuchapuza maendeleo kwa jamii husika.

Alieleza kuwa, serikali haiwezi kufanya kazi peke yake pasi na uwepo wa makundi ya aina hiyo ndani ya jamii, hivyo lazima mchango wao uoenekane.

Alifahamisha kuwa, asasi hizo zimekuwa zikiongoza makundi makubwa ya jamii, hivyo lazima viongozi wake wawe wabunifu na kuhakikisha wanatakeleza yale yaliyomo ndani ya Katiba zao.

“Tunajua na kuthamini vyema mchango wa NGOs, hivyo lazima ziendelee kuwa chachu ya kuisaidia serikali kuu, katika kufikia malengo yake kwa jamii”, alieleza.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba, ameipongeza ‘PACSO’ kwa kushirikiana kwa karibu na ofisi ya Mrajisi mkuu wa NGOs na kuhakikisha wanaifanyia marekebisho sheria ya asasi za kiraia.

Alifahamisha kuwa, hata rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alishatoa agizo la kufanyiwa marekebisho sheria zote zinazokwaza katika utendaji.

Mapema Mrajisi wa asasi za kiraia Zanzibar Ahmed Khalid Abdalla alisema, kazi ya kukusanya maoni ya wadau juu ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo, ilianza tokea mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema, maoni yaliokusanywa na wadau hao wa Unguja na Pemba, tayari yameshaandikwa pamoja na sasa hatua inayofuata ni kuyarejesha tena maoni hayo kwa wadau.

Alisema, kazi hiyo inayofanywa na PACSO kwa kushirikiana na ofisi yake chini ya ufadhili wa tasisi ya ‘PACT’ Tanzania, imekuwa mwafaka katika kufikia sheria yenye ubora.

Alieleza kuwa, malengo hasa ni kuwa na sheria bora, ambayo itafanya kazi kwa muda mrefu, bila ya kuwakwaza wadau ambao wengi wao ni wale wenye asasi za kiraia.

“Sheria ya Asasi ya Kiraia nambari 6 ya mwaka 1995, ilishapitwa na muda katika baadhi ya sehemu na vifungu vyake, ndio maana wadau wanataka kuifanyia marekebisho”, alieleza.

Mapema Katibu Mkuu wa PACSO Sifuni Ali Haji, akizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya ukumbi, alisema sheria hiyo ilikuwa na vifungu ambavyo vinakwaza kazi zao.

Alisema, moja ni kwa ofisi ya Pemba ya Mrajisi wa NGOs, kukosa uwezo wa kufanya uamuzi na usajili wa asasi za kiraia, jambo ambalo kwa sasa zilizoko Pemba, zinakabiliwa cha changamoto.

Hivyo amewataka wadau hao kuhakikisha wanatoa maoni yao, ili kuhakikisha sheria itakapopita inakuwa bora na inatekelezeka kwa wadau hao.

“Nafasi hii ni adhimu sana kwetu sisi wadau wa asasi za kiraia, maana sheria iliyokuwepo ilikuwa inatukwaza kwenye utendaji wetu, na hasa ilikuwa mamlaka makubwa aliyokuwa amepewa Mrajisi,’’alifafanua.

Baadhi ya wadau walisema, kama yaliomo kwenye msawada huo yatakwenda ngazi za juu na kupitishwa kama yalivyo, Zanzibar inaweza kuwa na sheria nzuri ya Asasi ya kiraia.

Mkutano huo wa siku mbili kwa wanaasasi za kiraia za Mkoa wa kusini Pemba, umeandaliwa na PACSO kwa kushirikiana na Ofisi ya Mrajisi kwa ufadhili wa tasisi wa PACT Tanzania.