PACSO yampongeza Dk; Hussein Ali Mwinyi kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa kampeni.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MTANDAO wa Asasi za Kiraia Pemba (PACSO) umempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk; Hussein Ali Mwinyi kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa kipindi cha kampeni.

Katibu wa PCSO Sifuni Ali Haji alisema, utekelezaji wa ahadi zake dk: Hussein Mwinyi umeipa matumaini makubwa mtandao huo pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kupatikana kwa huduma mbali mbali za kijamii bila ubaguzi.

Akitoa pongezi hizo kwa rais, katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Chake Chake Katibu huyo alisema, wanaamini kwamba dk: Mwinyi ni rais wa watu wote, rais wa wanyonge na ni kipenzi kikubwa cha wazanzibari, kwani kipindi cha miezi saba tu ya uongozi wake amefanya mambo makubwa.

Alisema kuwa, katika kipindi cha uongozi wake ameshatekeleza mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na  utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa bandari ya mafuta Mangapwani, kuanzisha wizara maalumu ya masuala ya uvuvi na uchumi wa buluu na hii ilitokana baada ya kufanya mkutano wake na wavuvi.

“Kipindi cha kampeni wavuvi waliomba kupatiwa Wizara maalumu na kwa kweli ameitimiza ahadi yake rais wetu kipenzi, tunajivunia na tunampongeza”, alisema.

Sifuni pia alimpongeza rais kwa kupunguza kodi na tozo ambazo zilikuwa ni kubwa na kero kwa wananchi na wafanyabiashara, kwani kwa sasa ada ya usafi inayotozwa na mabaraza ya miji ni 50,000/= kutoka 108,000/= ambayo ni sawa na ada ya shilingi 4,180 kwa siku.

Alisema, pia wanatoa pongezi kwa upatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya mzamzibari mkaazi, ambapo ni mafanikio makubwa kwani vinapatikana bila ya usumbufu.

“Tunatoa pongezi zetu za dhati kwa usimamiaji wa rasilimali za umma, kwani alitengua teuzi mbali mbali kwa sababu ya ubadhirifu mkubwa unaotendeka, ipo haja ya kupongezwa”, alisema Katibu huyo.

Katibu huyo alieleza, pia PACSO inampongeza dk: Mwinyi kwa kuanzisha mahakama maalumu ya udhalilishaji kwa watoto, kwani lengo lake ni kuona kwamba kesi hizo zinakwenda haraka ili haki ipatikane, kuondoa msongomano wa kesi katika mahakama za kawaida na kukomesha matendo ya udhalilishaji visiwani hapa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa PACSO Mohamed Ali Khamis alisema, pia wanampongeza ras Dk: Mwinyi kwa kuahidi kuwaweka pamoja wazaznzibari, jambo ambalo limeleta faraja kubwa kutokana na sasa jamii kuishi kwa amani na upendo bila kujali itikadi zao za vyama.

Mwenyekiti huyo alisema, wakati akiwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbali mbali, dk: Mwinyi aliagiza kufanywa marekebisho ya sheria zote ambazo zinakwamisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kijamii, jambo ambalo linawawezesha wao kuendesha mchakato wa sheria ya NGOs ya Zanzibar, ili kuziwezesha asasi za kiraia kufanya kazi kwa weledi mkubwa.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa PACSO Mohamed Najim Omar alimuomba Dk: Mwinyi kuendelea na msimamo wake wa utendaji, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatetea na kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

“Kitu chengine tunachomuomba ni namna gani fedha zilizopotea zinaweza kurejeshwa na hatua nyengine za kinidhamu ziweze kuchukuliwa”, alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha alimuomba rais azidi kutilia mkazo suala la udhibiti wa madawa ya kulevya kwa waingizaji, wauzaji na watumiaji, ili kuwakomboa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Mkurugenzi huyo pia alimuomba dk: Mwinyi kufanya kazi kwa karibu sana na asasi za kiraia, kwani zimekuwa ni daraja kubwa baina ya Serikali kuu na jamii katika masuala ya kimaendeleo na usimamiaji wa rasilimali za umma.

PACSO ni mtandao wa asasi za kiraia Pemba wenye Jumuiya wanachama 83 ambao pia ni mdau mkuu katika kufuatilia, kusikiliza, kuona, kushuhudia na hata kualikwa katika vikao mbali mbali vya utekelezaji vinavyofanywa na rais.