PACSO yafanya mkutano mkuu, yatoa angalizo kwa wanachama wake Pemba

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

JUMUIYA za kiraia kisiwani Pemba, zimetakiwa kufanya kazi kwa uwazi, ubunifu na mikakati ya kweli, ili kufikia ndoto zao za kuisaidia serikali kuu, katika mipango na mikakati ya maendeleo.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Mwenvuli wa asasi za kiraia kisiwani Pemba, PACSO Sifuni Ali Haji, alipokuwa akizungumza na wanaasasi hao, kwenye mkutano mkuu wa PACSO, uliofanyika skuli ya Maandalizi Madungu Chake Chake.

Alisema, asasi za kiraia zipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo endelevu wananchi kwa ujumla, kama ilivyo azma ya serikali kuu, katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Alieleza kuwa, asasi za kirai zimeanzishwa na wananchi wenyewe kwa hiari yao, sasa lazima zifanye kazi kwa uwazi, uwajibikaji na bila ya kutegemea wafadhili, kama zilivyo asasi nyingine.

Katibu Mkuu huyo alisema, PACSO ipo kwa ajili ya kuzijengea uwezo asasi hizo, ambao wanachama wake, ingawa nazo zinatakiwa kubuni mikakati yao wenyewe, kwa ajili ya kufanikisha ndoto zao.

“Kila asasi imeanzishwa ikiwa na katiba yake na mipango na mikakati yao, sasa lazima wafanye kama ilivyo kwenye katiba zao, na kufanya hivyo ni kusiadia serikali kuu”,alieleza.

Katika hatua nyingine, Katibu mkuu huyo wa PACSO amewataka wanaasasi hao, kuendelea kuyafanya kazi maagizo ya ofisi ya Mrajisi, ili kuzisajili kwa njia ya kielekroniki asasi zao.

Alisema, kama kuna changamoto yoyote ambayo inajitokeza kwa watendaji hao wa ofisi ya Mrajisi, wasisite kuwasiliana na ofisi ya PACSO, ili kuyafanyia kazi malalamiko yao.

Kwa upande wake Mratibu wa miradi kutoka PACSO Mohamed Najim Omar, wakati akiwasilisha utekelezaji wa kazi za PACSO kwa mwaka uliopita, alisema lazima asasi za kiraia, waitumie Ofisi ya PACSO, kwa ajili ya kubadilishana mawazo.

Alieleza kuwa, ofisi hiyo ipo kwa ajili yao, hivyo lazima waitumie ili kujua kinachoendelea na kutoa ushauri wao juu, ya namna ya kuiendeleza PACSO, badala ya kusubiri mkutano mkuu na kuto malalamiko.

“Ofisi ya PACSO ipo kwa ajili yetu, na lazima tujenge utamaduni wa kuitembelea kila wakati, ili kutoa mawazo na kubadilisha uzoefu,’’alieleza.

Mapema akifungua mkutano huo mkuu, Mwenyekiti wa Bodi ya PACSO Ali Mohamed Shela, aliwapongeza viongozi hao, kwa juhudi zao mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kuomba miradi kadhaa.

“Kwa sasa PACSO, inaendelea kumalizia utekelezaji wa mradi wa Ufuatiliaji wa rasilimali za umma ‘PETS’ na mradi huu umeleta matokeo mazuri, sasa lazima niwapongeze viongozi kwa ubunifu,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo, alizitaka asasi za kiraia ambazo hazijakamilisha taratibu za usajili kwa njia ya kisasa, kuharakisha, ili ziwe hai.

Aidha aliwataka viongozi wa asasi hizo, kulipa ada ya PACSO ili fedha zitakazopatikana, ziendelee kusaidia shughuli mbali mbali, ikiwa ni pamoja na gharama za kukodi ofisi.

Baadhi ya viongozi wa asasi za kiraia waliohudhuria mkutano huo, wamelalamika ofisi ya Mrajisi kwa kuwepo usumbufu mkubwa, wakati huu wanapofanya usajili wa kielektroniki.

Walisema, wamekuwa wakikwazwa na watendaji hao, kwa kuwacheleweshea usajili huo, jambo ambalo linalokatisha tamaa kuendelea kuwa na asasi hizo.

Mkutano huo mkuu wa PACSO uliridhia kuwa Mwenyekiti wa muda awe Mohamed Ali Mohamed, na Asha Msabah kuwa mjumbe mpya wa bodi ya wadhamini akichukua nafasi na mjumbe aliyepata uhamisho.