PACSO Pemba yazindua mradi wa aina yake

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MWEMVULI wa asasi za kiraia kisiwani Pemba PACSO, umekuja na mradi wa aina yake, unaokusudia kuwaelimisha wananchi njia bora na imara, za kufuatilia matumizi ya rasilimali fedha za umma, kwenye miradi ya ujenzi wa majengo ya skuli, inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Katibu mkuu wa PACSO Sifuni Ali Haji, alisema wananchi walio wengi hawana uwelewa na wapo wanaodhani kuwa, sio wajibu wao kuhoji, kufuatilia na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za umma, inapotekelezwa miradi ya maendeleo.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo wa kufuatilia mwenendo wa matumizi ya fedha za umma ‘PETS’ ukumbi wa mkitano Baraza la mji wa Chakechake, kwa masheha, madiwani, wanaasasi za kiraia wa wilaya ya Chakechake, alisema ni wajibu kwa wananchi, kufuatilia fedha hizo.

Alisema PACSO, baada ya kuona kuna kasoro kubwa ya wajibu huo kwa wananchi, na walio wengi kudhani kwamba kuna taasisi fulani, ndio yenye jukumu hilo, imeamua kuja na mradi huo ili kuwafumbua macho wananchi.

Alieleza kuwa, PACSO imedhamiria kutoa mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasimalia za umma, kwenye sekta ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pekee, hasa kwenye maeneo ya ujenzi.

“Kwa hatua hii, skuli ambazo zitapitiwa na mradi huu ni Madungu msingi, Vitongoji, Furaha, Vikunguni kwa wilaya ya Chakechake, Chambani na Kengeja kwa wilaya ya Mkoani,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, Katibu mkuu huyo wa PACSO, alisema mradi huo hauna nia ya kuingilia mipango, mikakati na dhamira njema ya serikali, bali ni kuwaelimisha wananchi na wadau wengine, juu ya wajibu wao wa kushiriki na kushirikishwa.

Hivyo amewaomba masheha, madiwani, maafisa wa mabaraza ya miji na wanaasasi za kiraia, kushirkiana vyema na PACSO, ili lengo la mradi huo lifikiwe.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo alisema, ushirikishwaji wa jamii ni mpango muhimu, katika kupanga, kulinda na kuchagua rasilimali za umma katika nchi kwa maslani ya taifa na watu wake.

Kwa upande wake, Mdhamini wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ZAECA kisiwani Pemba, Suleiman Ame Juma, alisema linalofanywa na PACSO ni sehemu ya utekelezaji wa sheria yao.

Alisema, kwenye kifungu cha 16 na 85 cha sheria yao no 1 ya mwaka 2012, ndio hasa sheria ya ZAECA imeeleza wazi wazi juu ya ushirikiano na taasisi nyingine, katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi ndani ya nchi.

Alisema, pamoja na kuwapongeza kwa kuibu mradi huo, lakini waelewe kwamba, wanakwenda kupambana na maslahi ya watu wachache, kwenye ujenzi wa mradi, kutokana na kutofuatwa sheria za manunuzi na majenzi zilivyo.

“Hili linalofanywa na PACSO, ni kubwa na mnatekeleza hata katiba zetu mbili, zinazowataka wananchi wazilinde rasilimali zao, maana mapambano haya yanahitaji nguvu za pamoja,’’alifafanua.

Aidha Mdhamini huyo, alisema kazi itakayofanywa na PACSO inaweza kuwasaidia wao, katika kufuatilia kisheria zaidi, iwapo watabaini miradi ya ujenzi ya wizara ya elimu, haikufuata taratibu au kuna ufujaji wa fedha.

Akiufafanua mradi huo, Mratibu wa mradi Mohamed Najim, alisema wadau wakuu  wa mradi huo ni Madiwani, Masheha, wanaasasi za kiraia, maafisa wa wizara elimu, baraza la mji, ofisi za wakuu wa wilaya, ZAECA, na kamati za skuli, ambao watautekeleza.

Miongoni wa shughuli zitakazofanywa juu ya mradi huo wa ufuatiliaji wa matumizi ya umma kwa jamii, ni mikutano, mafunzo juu ya kufahamu mbinu za kufuatilia fedha za umma, uundwaji wa kamati za ufuatiliaji na kufuatiwa na ukusanyaji wa takwimu na kuchambuliwa.

Aidha Mratibu huyo wa mradi kutoka PACSO Mohamed alisema, PETS ni mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma, ambapo mwananchi au kamati kufuatilia fedha za mradi kuanzia zinapotoka.

Alifafanua kuwa, kupitia mradi huo, wa miezi nane unaotarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani, wanatarajia ukimalizika utawajengea wananchi uwezo na ufahamu wa kufuatilia fedha za umma.

Baadhi ya walioshiriki kwenye uzinduzi wa mradi huo, wameutaka uongozi wa PACSO, kuwa makini na kuzikabili changamoto watakazokumbana nazo, wakati wa utekelezaji wa mradi.

Mradi huo wa mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma PETS, unaanza kutekelezwa na PACSO kuanzia mwezi Julai mwaka 2019  hadi mwezi Machi mwaka 2020, ukiwa na thamani ya shilingi milioni 60, utahusishwa ufuatiliaji wa majengo kwenye skuli za Madungu, Furaha, Vitongoji, Madungu msingi, Chambani na Kengeja .

Mwaka 2016, PACSO iliendesha mradi kama huo kwa kufuatilia ujenzi wa baraza kwenye wilaya za Wete na Micheweni na Mkoa wa kaskazini Pemba.

 

 

CHANZO: Pemba Today