PACSO mtaa kwa mtaa elimu ya mpiga kura Pemba

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA (pemba today)

JUMUIYA Mwemnvuli ya asasi za kiraia kisiwani Pemba ‘PACSO’ inaendelea na mchakato wa kutoa elimu ya mpiga kura, ambapo Oktoba 4, mwaka huu ilikuwa Micheweni na kuwataka wananchi wa eneo hilo, kutii maagizo yote ya tume za uchaguzi, ili kuepusha migogoro inayoepukika.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu mkuu wa ‘PACSO’ Pemba Sifuni Ali Haji alisema, tume imeweka kanuni kwa lengo la kulirahisisha zoezi la upigaji wa kura, kwenye uchaguzi mkuu wa vyama vingi unaotarajiwa kufayika Oktoba 28 mwaka huu.

Alisema, miongoni mwa kanuni za tume zote za uchaguzi, ni pamoja na wapiga kura kutovaa nguo zenye rangi ya chama au sare za vyama vyao, siku ya kupiga kura hasa eneo la kituoni.

Alisema, hilo limeonekana kama likfanyika linaweza kuzua migogoro, jambo ambalo linaweza kuepukwa na wafuasi na wagombea  wa vyama vya siasa.

Alisema, jengine ambalo wapiga kura wanapaswa kulizingatia na kutii, ni kuwa muda wa kupiga kura ukimalizika, muhusika atakaa nyuma ya mtu wa mwisho, na hatoruhusiwa mwengine baada ya muda huo.

“Kisheria vituo vya kupigia kura nchi nzima, vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na ikifika saa 10:00 jioni, itakuwa ndio mwisho wa kupokelewa kwa watakaowenda vituoni, hapo askari atakaa nyuma ya mtu wa mwisho,’’alifafanua.

Hata hivyo Katibu mkuu huyo wa PACSO, alisema kwa mujibu wa kanuni, kabla ya kuanza kupiga kura Msimamizi wa kituo atafungua masanduku ya kuhifadhia kura na kuwaonyesha mawakala wa vyama na watu wengine.

“Hili lilionenakana linaweza kuzua wasi wasi, na ndio maana kanuni ikaelekeza hivyo, ili mawakala wa vyama na watu wengine walioruhusiwa kuwepo, wajiridhishe kuwa ndani ya sanduku hilo hamna kitu,’’alifafanua.

Hata hivyo, amewakumbusha wananchi hao kuwa, siku ya kupiga kura itakuwa ni Oktoba 28, mwaka huu na kuwataka wafike mapema vituoni na kufuata maelekezo.

Nae mjumbe wa PACSO Robert Miguwa Ndalami aliwakumbusha wananchi hao kuwa, hata suala la mgombea au gari za chama kusafirisha wapiga kura, ni kosa.

Aidha alisema kwa mujibu wa kununi za tume za uchaguzi, hairuhusiwi kwa mtu mmoja, kumsaidia mtu zaidi ya mmoja katika upigaji wa kura.

“Inawezekana wapo wananchi wenzetu wameshajipanga kuwapigia kura watu zaidi ya wawili, hali lazima tulielewe mapema kuwa, haliruhusiki ukishampigia mmoja nawe piga ya kwako urudi nyumbani,’’alieleza.

Nae Haroub Mmanga Simai, aliwaeleza wananchi hao kuwa, kutokana na tume kujali makundi mbali mbali, imeweka utaratibu kwa wazee, wenye ulemavu, wagonjwa, wajawazito na wenye watoto wachanga, kupewa kipaumbele.

“Tusije tukaanzisha misuguano, akitokezea mzee au mwenye mtoto mchanga tukamuona anaingia moja kwa moja ndani ya kituo cha kupigia kura, kanuni zimewahurumia,’’alifafanua.

Mwenyekiti wa wazee wilaya ya Micheweni Shaame Khatib Hamad alisema, PACSO imefanya jambo jema kuwafikia na kuwaelimisha, juu ya mpango huo.

Alisema, awali waliona kama jambo la kisheria kwa wagombea kuwasafirisha wagonjwa na wasiojiweza kuwapeleka vituoni kwa ajili ya upigaji wa kura.

Mapema sheha wa shehia ya Majenzi Jimbo la Micheweni, Faki Kombo Hamad, alisema sasa wananchi wake wamepata mwamko na kuahidi elimu waliyoipata kuisambaaza kwa wengine.

“Tuliowengi tulidhani kuwa, unaweza kumsaidia watu kupiga kura hata watano kama wapo, lakini kwa mkutano huu ulioitishwa na wenzetu wa PACSO, sasa tumeelewa kwa huzidi mtu mmoja kumsaidia,’’alifafanua.

Mtandao wa asasi za kiraia kisiwani Pemba ‘PACSO’ ni moja ya asasi ambazo zilizopewa kibali cha tume ya uchaguzi cha kutoa elimu ya mpiga kura, na tayari wameshawafiki wananchi wa Mtambile, Wawi, Kibokoni, Micheweni, Gombani, Vitongoji kwa wastani wa wananchi 1500 wameshafikiwa.