JAMII YAKUMBUSHWA KUILINDA HAKI KUU YA BINAADAMU
JAMII imekumbushwa kuwa, moja ya haki kuu ya msingi kwa kila mwanadamu ni ile ya kuishi, hivyo ni kosa kwa mtu mwengine yeyote kumuondolea mwenzake.
Hayo yalielezwa na mtoa mada mwanasheria kutoka Shirika la Msaada na Haki za Binaadamu Siti Habib Mohamed, wakati akiendesha mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari, wadau wa habari na wasaidizi wa sheria, yanayofanyika Chuo cha Amali Vitongoji Chake chake na kuandaliwa na Mwemvuli wa asasi za Kirai Pemba PACSO kwa ufadhili wa UNDP.
Alisema kua zana ya haki za binadamu ilianzishwa mnamo mwaka 1948 baada ya vita vya kwanza vya dunia, hivyo ni wajibu wa kila mmoja hadi leo hii, kuhakikisha anailinda na kuitetea haki ya kuishi ya mwanzake.
Alieleza kuwa, haki za binadamu kimsingi ni yale madai au haki zote ambazo anadai binamu mara baada ya kuzaliwa, na kwa kawida hakuna taasisi yoyote ambayo inaweza kuzuia.
‘’Ni kweli haki ya msingi kwa kila mwanadamu ni ile ya kuishi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anailinda yake mwenyewe na mwenzake,’’anaelkeza.
Hata hivyo alieleza kua kupitia Mkataba wahaki za binadamu ambao uliasisiwa mwaka 1966 na kuanza kufanyaka kazi mwaka 1976, umeanisha haki nyingine kadhaa za binadamu kama vile kutoa maoni.
Katika hatua nyingine mtoa mada huyo alieleza kua zipo hatua mbali mbali, ambazo zimekuja kwa ajili ya kuzilinda haki hizo ikiwa ni pamoja na kuanzishwa wizara maalum, kuanzishwa kwa tume ya Haki za binadamu na utawala bora.
‘’Lakini hata kuingizwa kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile ya Zanzibar ya mwaka 1894 na uwepo wa wizara husika na asasi ni sehemu ya kuzilinda,’’alifafanua.
Mapema Mkurugenzi wa PACSO Mohamed Najim Omar, alisema waliona wakutane na waandishi wa habari, wanaharakati wa haki za binadamu na wasaidizi wa sheria, ili kuwajengea uwezo.
‘’Waandishi wananafasi kubwa ya kuhakikisha wanakemea matendo ya uvunjifu wa haki za binadamu kupitia kazi zao,’’alieleza.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema bado elimu inahitajika kwa jamii, ili wafahamu athari za uvunjifu wa haki za binadamu.
Mshiriki kutoka chama cha ACT Wazalendo Saleh Nassor Juma, waliishukuru taasisi hii ya PACSO kwa kuwapa mafunzo hayo, ambayo yamewapa uwelewa zaidi.
Nae mtaangazaji wa Redio Istiqama Pemba Bakar Khamis Juma, alisema kama mataifa makubwa, yatajenga utamaduni wa kuziheshimu haki za binadamu dunia itakuwa salama.
Nao washiriki Abubakar Mohamed Ali ,Mwache Juma Abdalla walisema, kama vyombo vya habari vitakuwa huru kufanya kazi, wanaweza kukemea matendo ya uvunjifu wa haki za binadamu yanayojitokeza.
Mratibu wa miradi kutoka Shirika la Maendeleo Ulimwenguni la UNDP Gamalick Sun alisema wataendelea kuiunga mkono PACSO katika shughuli zao mbali mbali.
Alieleza kuwa, anaamini PACSO ni sehemu ya uwakilishi wa wananchi, na ndio maana hata mafunzo hayo yamewashirikisha watu wa kada mbali mbali.
Mafunzo hayo ya siku nne mada kadhaa zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza, haki za binaadamu, majukumu ya waandishi wa habari na jukumu la jamii katika kulinda haki za binaadamu,.