16 Dec, 2021

PACSO: Yawanyooshea kidole wanaume vizingiti kwa wanawake kumiliki mali

MTANDAO wa Asasi wa Kiraia Pemba ‘PACSO’ umesema hakuna kanuni, sera, sheria wala mkataba wowote wa kitaifa, kikanda na wa kimataifa, unaomzuia mwanamke kutomiliki mali, bali kinachofanyika na kutengenezewa vikwazo na baadhi ya wanaume.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa mtandao huo, Mohamed Ali Khamis, wakati alipokuwa akifungua kongamano la siku moja la wanawake, kumiliki rasilimali lililoandaliwa na PACSO kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, kupitia shirika la misaada la ‘IRISH AID’ na kufanyika Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake.

Alisema, kama wanaume ambao ndio wanaoaminiwa na wanawake wataendelea kuzikalia haki za wanaweke, kundi hilo litaendelea kusikia kwenye vyombo vya habari, suala la umiliki wa rasilimali.

Mwenyekti huyo alisema, majukwaa kama hayo wakati mwengine huwasaidia wanawake kuwazindua na kupata uwelewa wa kuweza kudai haki zao mbali mbali.

“Wanawake wanahaki pia ya kumiliki rasilimali kama vile ardhi, lakini sasa kama wanaume hawakuwa tayari kujivua gamba, haki hiyo itaishia kwenye karatasi pekee,’’alieleza.

Mapema Mratibu wa miradi kutoka ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, alisema mradi huo ambao ni wa miezi miwili, unamalengo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kongamano kama hilo.

Shughuli nyingine wanayotarajia kuifanya, ni mafunzo kwa jamii juu ya elimu ya ushawishi na utetezi, wa masuala ya kumiliki rasilimali kwa wanawake.

Aidha Mratibu huyo alifafanua kuwa, pia wanatarajia kuwafunza wananchi masuala ya sheria na kanuni za ardhi, ili wapate uwelewa.

“Ni kweli kwenye suala la sheria za ardhi nako kuna mambo kadhaa, lakini ndani ya utekelezaji wa mradi huu, wananchi wakiwemo wanawake, watafunzwa sheria hizo,’’alieleza.

Akiwasilisha mada ya haki umiliki wa ardhi kwa wanawake, Kaimu Mratibu wa Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba, Safia Saleh Sultan, alisema changamoto kubwa moja ni urasimu wa umiliki wa ardhi.

Jengine alisema, wanawake waliowengi hawana uwelewa mpana wa masuala ya sheria ya ardhi, hali inayopelekea kupoteza umiliki wa matumizi kwa njia rahisi.

Wakichangia mada hiyo wanakongamano hilo, walishauri elimu zaidi itolewe hasa kwa wanawake walioko vijijini, ambako ndio kwenye migogoro mingi ya ardhi.

Said Amour Juma wa Wawi, alisema kubwa zaidi la kuangalia ni uwelewa wa wananchi ikiwa uko vizuri, kwenye suala la umiliki.

Nuru Ali Nassor alisema, kwa vile suala la ucheleweshaji mirathi huchangia wanawake kukosa umiliki, ni vyema jamii ikafuata maelekezo ya kurithi kwa wakati.

Kwa upande wake, Shikha Kitwana Sururu, aliziomba mamlaka husika, kuwasaidia zaidi wanawake hasa wanyonge ili wasipoteze haki zao za umiliki.

Hata hivyo mshiriki Fatma Khamis Juma, alipendekeza liwepo somo maalum la urithi kuanzia elimu ya msingi, ili jambo hilo lifahamike vyema ndani ya jamii.

“Lakini hata suala la ushirikina uliyopo ndani ya jamii na vitisho vya wanaume, wakati mwengine, huwa unatujenga woga sisi kudai haki zetu mfano za urithi,’’alifafanua Zamzam Khamis Saburi wa Kengeja.

Mradi huo wa kuwajengea uwezo wanawake kuweza kudai rasilimali zao kama vile ardhi, ni wa miezi miwili unatekelezwa na PACSO kwa ufadhili wa shirika la misaada la Ireland ‘IRISH AID’.

27 May, 2021

PACSO yampongeza Dk; Hussein Ali Mwinyi kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa kampeni.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MTANDAO wa Asasi za Kiraia Pemba (PACSO) umempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk; Hussein Ali Mwinyi kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa kipindi cha kampeni.

Katibu wa PCSO Sifuni Ali Haji alisema, utekelezaji wa ahadi zake dk: Hussein Mwinyi umeipa matumaini makubwa mtandao huo pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kupatikana kwa huduma mbali mbali za kijamii bila ubaguzi.

Akitoa pongezi hizo kwa rais, katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Chake Chake Katibu huyo alisema, wanaamini kwamba dk: Mwinyi ni rais wa watu wote, rais wa wanyonge na ni kipenzi kikubwa cha wazanzibari, kwani kipindi cha miezi saba tu ya uongozi wake amefanya mambo makubwa.

Alisema kuwa, katika kipindi cha uongozi wake ameshatekeleza mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na  utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa bandari ya mafuta Mangapwani, kuanzisha wizara maalumu ya masuala ya uvuvi na uchumi wa buluu na hii ilitokana baada ya kufanya mkutano wake na wavuvi.

“Kipindi cha kampeni wavuvi waliomba kupatiwa Wizara maalumu na kwa kweli ameitimiza ahadi yake rais wetu kipenzi, tunajivunia na tunampongeza”, alisema.

Sifuni pia alimpongeza rais kwa kupunguza kodi na tozo ambazo zilikuwa ni kubwa na kero kwa wananchi na wafanyabiashara, kwani kwa sasa ada ya usafi inayotozwa na mabaraza ya miji ni 50,000/= kutoka 108,000/= ambayo ni sawa na ada ya shilingi 4,180 kwa siku.

Alisema, pia wanatoa pongezi kwa upatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya mzamzibari mkaazi, ambapo ni mafanikio makubwa kwani vinapatikana bila ya usumbufu.

“Tunatoa pongezi zetu za dhati kwa usimamiaji wa rasilimali za umma, kwani alitengua teuzi mbali mbali kwa sababu ya ubadhirifu mkubwa unaotendeka, ipo haja ya kupongezwa”, alisema Katibu huyo.

Katibu huyo alieleza, pia PACSO inampongeza dk: Mwinyi kwa kuanzisha mahakama maalumu ya udhalilishaji kwa watoto, kwani lengo lake ni kuona kwamba kesi hizo zinakwenda haraka ili haki ipatikane, kuondoa msongomano wa kesi katika mahakama za kawaida na kukomesha matendo ya udhalilishaji visiwani hapa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa PACSO Mohamed Ali Khamis alisema, pia wanampongeza ras Dk: Mwinyi kwa kuahidi kuwaweka pamoja wazaznzibari, jambo ambalo limeleta faraja kubwa kutokana na sasa jamii kuishi kwa amani na upendo bila kujali itikadi zao za vyama.

Mwenyekiti huyo alisema, wakati akiwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbali mbali, dk: Mwinyi aliagiza kufanywa marekebisho ya sheria zote ambazo zinakwamisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kijamii, jambo ambalo linawawezesha wao kuendesha mchakato wa sheria ya NGOs ya Zanzibar, ili kuziwezesha asasi za kiraia kufanya kazi kwa weledi mkubwa.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa PACSO Mohamed Najim Omar alimuomba Dk: Mwinyi kuendelea na msimamo wake wa utendaji, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatetea na kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

“Kitu chengine tunachomuomba ni namna gani fedha zilizopotea zinaweza kurejeshwa na hatua nyengine za kinidhamu ziweze kuchukuliwa”, alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha alimuomba rais azidi kutilia mkazo suala la udhibiti wa madawa ya kulevya kwa waingizaji, wauzaji na watumiaji, ili kuwakomboa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Mkurugenzi huyo pia alimuomba dk: Mwinyi kufanya kazi kwa karibu sana na asasi za kiraia, kwani zimekuwa ni daraja kubwa baina ya Serikali kuu na jamii katika masuala ya kimaendeleo na usimamiaji wa rasilimali za umma.

PACSO ni mtandao wa asasi za kiraia Pemba wenye Jumuiya wanachama 83 ambao pia ni mdau mkuu katika kufuatilia, kusikiliza, kuona, kushuhudia na hata kualikwa katika vikao mbali mbali vya utekelezaji vinavyofanywa na rais.

26 May, 2021

MKUTANO WA KUKABIDHI RASIMU YA ASASI ZA KIRAIA KWA MWENYEKITI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA ZANZIBAR

Mkurugenzi wa mtandao wa asasi za kiraia Pemba (PACSO) Nd. Mohamed Najim Omar kwa pamoja na Nd. Sifuni Ali Haji (katibu) wamekabidhi rasimu ya asasi za kiraia Zanzibar kwa mwenyekiti wa Tume ya kurekebisho sheria Zanzibar  Ndugu khadija Shamte.

Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa ZSSF kilimani Zanzibar tarehe 26/05/2021.

Mrajisi wa asasi za kiraia Zanzibar, Nd. Ahmed Khalid Abdullah akimkaribisha mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar.

 

Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar Ndugu khadija Shamte (watatu kutoka kulia) akitoa neno.

 

20 Mar, 2021

SALAMU ZA RAMBIRAMBI

MTANDAO wa Asasi za Kiraia Pemba (PACSO) tunatoa salamu za rambirambi kwa familia ya  mjane wa Hayati, Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli, watoto, ndugu na jamaa kwa  kuondokewa na mpendwa wao na wananchi wote wa Tanzania kwa pigo hili kubwa.

Ni msiba mzito ambao hatukutarajia, sote tunafahamu jinsi Hayati, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alivyoipenda nchi, alivyowapenda Watanzania na kujitoa kwa watu wake kwa dhamira ya dhati na nia njema ya kuibadilisha taswira ya nchi yake.

“Tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa Bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli, Mhe. Magufuli alikuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yetu na Africa kwa ujumla”

5 Mar, 2021

Mrajisi aipa tano PACSO marekebisho sheria ya NGOs

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MRAJISI wa Jumuia zisizo za serikali Zanzibar Ahmed Khalid Abdalla, ameupongeza Mwenvuli wa Jumuiya za Kiraia Pemba ‘PACSO’ kwa juhudi zake mbali mbali, katika kuhakikisha asasi za kiraia zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Mrajisi huyo aliyasema hayo ukumbi wa kiwanda cha Mafuta ya makonyo Wawi Chake chake, alipokuwa akizungumza na wanaasasi hao wa Mkoa wa kusini Pemba, kwenye mkutano wa siku mbilim wa kuwasilisha msawada wa sheria wa Jumuia za kiraia Zanzibar.

Alisema ‘PACSO’ imekuwa mdau mkubwa katika kuipigia kelele sheria ya sasa ya asasi ya kiraia nambari 6 ya mwaka 1995, ambapo kwa, imeonekana kupitwa na muda wake.

Alieleza kuwa, harakati za ‘PACSO’ za kuhakikisha sheria hiyo inafanyiwa marekebisho, imeaisaidia sana ofisi ya Mrajisi, kwani sheria hiyo wenyewe ni wadau wa asasi hizo.

“Sisi Ofisi ya Mrajisi wa asasi za kiraia, tunapongeza sana mchango wa PACSO, na wafadhili wake kuanzia PACT- Tanzania hadi wale ‘the foundation for civil society’, kwa kuandaa mchakato wa marekebisho ya sheria hii,’’alieleza.

Katika hatua nyingine Mrajisi huyo, alisema baada ya mchakato wa mwanzo wa kukusanya maoni ya wadau, juu ya marekebisho hayo, yaliofanywa na PACSO, sasa ndio tayari kumeshapatikana kwa mswaada wa sheria hiyo.

Hata hivyo, aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuendelea kutoa maoni yao, kupitia PACSO na ofisi ya Mrajisi, kabla ya mswaada wa sheria hiyo kufikishwa ngazi ya makatibu wakuu.

Mapema akiwasilisha mswada wa sheria ya asasi za kiraia Zanzibar, mwanasheria Salum Mohamed Abdalla, alisema sheria hiyo, haiwezi kuingizwa kila kitu, kwani baadae hufuatwa na sera na kanuni.

Aidha alisema sheria hiyo, ni miongoni mwa sheria ambayo imewashirikisha wadau kuanzia mwanzo hadi mwisho, na huwenda baada ya kupitishwa ikadumu kwa muda mrefu.

Wakitoa maoni yao, juu ya mswada wa sheria hiyo, wanaasasi hao za kiria za mkoa wa kusini Pemba, wamesema sheria hiyo ni nzuri na ina iweza kuwa mfano wa kupatikana kwa sheria bora.

Khalifan Amour Mohamed, alisema sheria hiyo ni nzuri ikiwa kama itakwenda na kukubaliwa kama ilivyo sasa, kutokana na kutoa haki kwa pande zote.

Alisema, kama Mrajisi amewekewa sifa za kuwa na uwelewa na asasi za kiraia, lakini hata Mwenyrkiti wa bodi, lazima sifa kama hizo awe nazo katika kuendesha bodi hiyo.

Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya PACSO Ali Mohamed Shela, alisema lazima sheria hiyo ieleze kila kitu, kwani inatakiwa idumu kwa miaka kadhaa ijayo, na sio kuwa na sheria ambayo baada ya muda mfupi inakwaza.

Awali Mkurugenzi wa ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, aliwataka wajumbe hao, kuhakikisha wanaitumia vyema fursa hiyo, ili maoni yao yawe chachu ya kupata sheria bora.

Mapema Katibu Mkuu wa PACSO Sifuni Ali Haji, akizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya ukumbi, alisema sheria hiyo ilikuwa na vifungu ambavyo vinakwaza kazi zao.

Alisema, moja ni kwa ofisi ya Pemba ya Mrajisi wa NGOs, kukosa uwezo wa kufanya uamuzi na usajili wa asasi za kiraia, jambo ambalo kwa sasa zilizoko Pemba, zinakabiliwa cha changamoto.

Mkutano huo wa siku mbili ni muendelezo wa mkutano wa kwanza, uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, ambao wanaasasi za Pemba, walitoa maoni ya awali ya marekebisho ya sheria hiyo.