27 May, 2021

PACSO yampongeza Dk; Hussein Ali Mwinyi kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa kampeni.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MTANDAO wa Asasi za Kiraia Pemba (PACSO) umempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk; Hussein Ali Mwinyi kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa kipindi cha kampeni.

Katibu wa PCSO Sifuni Ali Haji alisema, utekelezaji wa ahadi zake dk: Hussein Mwinyi umeipa matumaini makubwa mtandao huo pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kupatikana kwa huduma mbali mbali za kijamii bila ubaguzi.

Akitoa pongezi hizo kwa rais, katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Chake Chake Katibu huyo alisema, wanaamini kwamba dk: Mwinyi ni rais wa watu wote, rais wa wanyonge na ni kipenzi kikubwa cha wazanzibari, kwani kipindi cha miezi saba tu ya uongozi wake amefanya mambo makubwa.

Alisema kuwa, katika kipindi cha uongozi wake ameshatekeleza mambo mbali mbali ikiwa ni pamoja na  utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa bandari ya mafuta Mangapwani, kuanzisha wizara maalumu ya masuala ya uvuvi na uchumi wa buluu na hii ilitokana baada ya kufanya mkutano wake na wavuvi.

“Kipindi cha kampeni wavuvi waliomba kupatiwa Wizara maalumu na kwa kweli ameitimiza ahadi yake rais wetu kipenzi, tunajivunia na tunampongeza”, alisema.

Sifuni pia alimpongeza rais kwa kupunguza kodi na tozo ambazo zilikuwa ni kubwa na kero kwa wananchi na wafanyabiashara, kwani kwa sasa ada ya usafi inayotozwa na mabaraza ya miji ni 50,000/= kutoka 108,000/= ambayo ni sawa na ada ya shilingi 4,180 kwa siku.

Alisema, pia wanatoa pongezi kwa upatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya mzamzibari mkaazi, ambapo ni mafanikio makubwa kwani vinapatikana bila ya usumbufu.

“Tunatoa pongezi zetu za dhati kwa usimamiaji wa rasilimali za umma, kwani alitengua teuzi mbali mbali kwa sababu ya ubadhirifu mkubwa unaotendeka, ipo haja ya kupongezwa”, alisema Katibu huyo.

Katibu huyo alieleza, pia PACSO inampongeza dk: Mwinyi kwa kuanzisha mahakama maalumu ya udhalilishaji kwa watoto, kwani lengo lake ni kuona kwamba kesi hizo zinakwenda haraka ili haki ipatikane, kuondoa msongomano wa kesi katika mahakama za kawaida na kukomesha matendo ya udhalilishaji visiwani hapa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa PACSO Mohamed Ali Khamis alisema, pia wanampongeza ras Dk: Mwinyi kwa kuahidi kuwaweka pamoja wazaznzibari, jambo ambalo limeleta faraja kubwa kutokana na sasa jamii kuishi kwa amani na upendo bila kujali itikadi zao za vyama.

Mwenyekiti huyo alisema, wakati akiwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbali mbali, dk: Mwinyi aliagiza kufanywa marekebisho ya sheria zote ambazo zinakwamisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kijamii, jambo ambalo linawawezesha wao kuendesha mchakato wa sheria ya NGOs ya Zanzibar, ili kuziwezesha asasi za kiraia kufanya kazi kwa weledi mkubwa.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa PACSO Mohamed Najim Omar alimuomba Dk: Mwinyi kuendelea na msimamo wake wa utendaji, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatetea na kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

“Kitu chengine tunachomuomba ni namna gani fedha zilizopotea zinaweza kurejeshwa na hatua nyengine za kinidhamu ziweze kuchukuliwa”, alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha alimuomba rais azidi kutilia mkazo suala la udhibiti wa madawa ya kulevya kwa waingizaji, wauzaji na watumiaji, ili kuwakomboa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Mkurugenzi huyo pia alimuomba dk: Mwinyi kufanya kazi kwa karibu sana na asasi za kiraia, kwani zimekuwa ni daraja kubwa baina ya Serikali kuu na jamii katika masuala ya kimaendeleo na usimamiaji wa rasilimali za umma.

PACSO ni mtandao wa asasi za kiraia Pemba wenye Jumuiya wanachama 83 ambao pia ni mdau mkuu katika kufuatilia, kusikiliza, kuona, kushuhudia na hata kualikwa katika vikao mbali mbali vya utekelezaji vinavyofanywa na rais.

20 Mar, 2021

SALAMU ZA RAMBIRAMBI

MTANDAO wa Asasi za Kiraia Pemba (PACSO) tunatoa salamu za rambirambi kwa familia ya  mjane wa Hayati, Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli, watoto, ndugu na jamaa kwa  kuondokewa na mpendwa wao na wananchi wote wa Tanzania kwa pigo hili kubwa.

Ni msiba mzito ambao hatukutarajia, sote tunafahamu jinsi Hayati, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alivyoipenda nchi, alivyowapenda Watanzania na kujitoa kwa watu wake kwa dhamira ya dhati na nia njema ya kuibadilisha taswira ya nchi yake.

“Tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa Bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli, Mhe. Magufuli alikuwa chachu ya maendeleo kwa nchi yetu na Africa kwa ujumla”

5 Mar, 2021

Mrajisi aipa tano PACSO marekebisho sheria ya NGOs

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MRAJISI wa Jumuia zisizo za serikali Zanzibar Ahmed Khalid Abdalla, ameupongeza Mwenvuli wa Jumuiya za Kiraia Pemba ‘PACSO’ kwa juhudi zake mbali mbali, katika kuhakikisha asasi za kiraia zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Mrajisi huyo aliyasema hayo ukumbi wa kiwanda cha Mafuta ya makonyo Wawi Chake chake, alipokuwa akizungumza na wanaasasi hao wa Mkoa wa kusini Pemba, kwenye mkutano wa siku mbilim wa kuwasilisha msawada wa sheria wa Jumuia za kiraia Zanzibar.

Alisema ‘PACSO’ imekuwa mdau mkubwa katika kuipigia kelele sheria ya sasa ya asasi ya kiraia nambari 6 ya mwaka 1995, ambapo kwa, imeonekana kupitwa na muda wake.

Alieleza kuwa, harakati za ‘PACSO’ za kuhakikisha sheria hiyo inafanyiwa marekebisho, imeaisaidia sana ofisi ya Mrajisi, kwani sheria hiyo wenyewe ni wadau wa asasi hizo.

“Sisi Ofisi ya Mrajisi wa asasi za kiraia, tunapongeza sana mchango wa PACSO, na wafadhili wake kuanzia PACT- Tanzania hadi wale ‘the foundation for civil society’, kwa kuandaa mchakato wa marekebisho ya sheria hii,’’alieleza.

Katika hatua nyingine Mrajisi huyo, alisema baada ya mchakato wa mwanzo wa kukusanya maoni ya wadau, juu ya marekebisho hayo, yaliofanywa na PACSO, sasa ndio tayari kumeshapatikana kwa mswaada wa sheria hiyo.

Hata hivyo, aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuendelea kutoa maoni yao, kupitia PACSO na ofisi ya Mrajisi, kabla ya mswaada wa sheria hiyo kufikishwa ngazi ya makatibu wakuu.

Mapema akiwasilisha mswada wa sheria ya asasi za kiraia Zanzibar, mwanasheria Salum Mohamed Abdalla, alisema sheria hiyo, haiwezi kuingizwa kila kitu, kwani baadae hufuatwa na sera na kanuni.

Aidha alisema sheria hiyo, ni miongoni mwa sheria ambayo imewashirikisha wadau kuanzia mwanzo hadi mwisho, na huwenda baada ya kupitishwa ikadumu kwa muda mrefu.

Wakitoa maoni yao, juu ya mswada wa sheria hiyo, wanaasasi hao za kiria za mkoa wa kusini Pemba, wamesema sheria hiyo ni nzuri na ina iweza kuwa mfano wa kupatikana kwa sheria bora.

Khalifan Amour Mohamed, alisema sheria hiyo ni nzuri ikiwa kama itakwenda na kukubaliwa kama ilivyo sasa, kutokana na kutoa haki kwa pande zote.

Alisema, kama Mrajisi amewekewa sifa za kuwa na uwelewa na asasi za kiraia, lakini hata Mwenyrkiti wa bodi, lazima sifa kama hizo awe nazo katika kuendesha bodi hiyo.

Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya PACSO Ali Mohamed Shela, alisema lazima sheria hiyo ieleze kila kitu, kwani inatakiwa idumu kwa miaka kadhaa ijayo, na sio kuwa na sheria ambayo baada ya muda mfupi inakwaza.

Awali Mkurugenzi wa ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar, aliwataka wajumbe hao, kuhakikisha wanaitumia vyema fursa hiyo, ili maoni yao yawe chachu ya kupata sheria bora.

Mapema Katibu Mkuu wa PACSO Sifuni Ali Haji, akizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya ukumbi, alisema sheria hiyo ilikuwa na vifungu ambavyo vinakwaza kazi zao.

Alisema, moja ni kwa ofisi ya Pemba ya Mrajisi wa NGOs, kukosa uwezo wa kufanya uamuzi na usajili wa asasi za kiraia, jambo ambalo kwa sasa zilizoko Pemba, zinakabiliwa cha changamoto.

Mkutano huo wa siku mbili ni muendelezo wa mkutano wa kwanza, uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, ambao wanaasasi za Pemba, walitoa maoni ya awali ya marekebisho ya sheria hiyo.

3 Mar, 2021

RC kusini Pemba atoa neno kwa NGOs

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema uwepo wa asasi nyingi za kiraia nchini, iwe ni chachu ya kuchapuza maendeleo ya nchi na hayo yatajitokeza iwapo zitafanya kazi kwa bidii.

Mkuu huyo wa mkoa, aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa mkutano wa kuwasilisha rasimu ya mswada wa sheria ya Jumuiya zisizo za serikali nambari 6 ya mwaka 1995, mkutano ulioandaliwa na mwenvuli wa asasi za kiraia Pemba, ‘PACSO’ ambao umefanyika kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake.

Alisema, serikali inathamini kwa kiasi kikubwa, mchango wa NGOs, hivyo uwepo wake kwa wingi nchini, iwe sababu ya kuchapuza maendeleo kwa jamii husika.

Alieleza kuwa, serikali haiwezi kufanya kazi peke yake pasi na uwepo wa makundi ya aina hiyo ndani ya jamii, hivyo lazima mchango wao uoenekane.

Alifahamisha kuwa, asasi hizo zimekuwa zikiongoza makundi makubwa ya jamii, hivyo lazima viongozi wake wawe wabunifu na kuhakikisha wanatakeleza yale yaliyomo ndani ya Katiba zao.

“Tunajua na kuthamini vyema mchango wa NGOs, hivyo lazima ziendelee kuwa chachu ya kuisaidia serikali kuu, katika kufikia malengo yake kwa jamii”, alieleza.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba, ameipongeza ‘PACSO’ kwa kushirikiana kwa karibu na ofisi ya Mrajisi mkuu wa NGOs na kuhakikisha wanaifanyia marekebisho sheria ya asasi za kiraia.

Alifahamisha kuwa, hata rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alishatoa agizo la kufanyiwa marekebisho sheria zote zinazokwaza katika utendaji.

Mapema Mrajisi wa asasi za kiraia Zanzibar Ahmed Khalid Abdalla alisema, kazi ya kukusanya maoni ya wadau juu ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo, ilianza tokea mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema, maoni yaliokusanywa na wadau hao wa Unguja na Pemba, tayari yameshaandikwa pamoja na sasa hatua inayofuata ni kuyarejesha tena maoni hayo kwa wadau.

Alisema, kazi hiyo inayofanywa na PACSO kwa kushirikiana na ofisi yake chini ya ufadhili wa tasisi ya ‘PACT’ Tanzania, imekuwa mwafaka katika kufikia sheria yenye ubora.

Alieleza kuwa, malengo hasa ni kuwa na sheria bora, ambayo itafanya kazi kwa muda mrefu, bila ya kuwakwaza wadau ambao wengi wao ni wale wenye asasi za kiraia.

“Sheria ya Asasi ya Kiraia nambari 6 ya mwaka 1995, ilishapitwa na muda katika baadhi ya sehemu na vifungu vyake, ndio maana wadau wanataka kuifanyia marekebisho”, alieleza.

Mapema Katibu Mkuu wa PACSO Sifuni Ali Haji, akizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya ukumbi, alisema sheria hiyo ilikuwa na vifungu ambavyo vinakwaza kazi zao.

Alisema, moja ni kwa ofisi ya Pemba ya Mrajisi wa NGOs, kukosa uwezo wa kufanya uamuzi na usajili wa asasi za kiraia, jambo ambalo kwa sasa zilizoko Pemba, zinakabiliwa cha changamoto.

Hivyo amewataka wadau hao kuhakikisha wanatoa maoni yao, ili kuhakikisha sheria itakapopita inakuwa bora na inatekelezeka kwa wadau hao.

“Nafasi hii ni adhimu sana kwetu sisi wadau wa asasi za kiraia, maana sheria iliyokuwepo ilikuwa inatukwaza kwenye utendaji wetu, na hasa ilikuwa mamlaka makubwa aliyokuwa amepewa Mrajisi,’’alifafanua.

Baadhi ya wadau walisema, kama yaliomo kwenye msawada huo yatakwenda ngazi za juu na kupitishwa kama yalivyo, Zanzibar inaweza kuwa na sheria nzuri ya Asasi ya kiraia.

Mkutano huo wa siku mbili kwa wanaasasi za kiraia za Mkoa wa kusini Pemba, umeandaliwa na PACSO kwa kushirikiana na Ofisi ya Mrajisi kwa ufadhili wa tasisi wa PACT Tanzania.

17 Feb, 2021

PACSO yamaliza mradi wa PETS, yagundua mazuri, mabaya fedha za umma

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAPO walionadhani kuwa, suala la ufuatiliaji wa rasilima za umma ‘PETS’ wala wananchi haliwahusu kamwe.

Wakidhani kuwa, hilo ni jukumu la serikali kuu pekee, na hasa kwa vile rasilima hizo iwe fedha au vitu vyengine, vimetolewa na serikali yenyewe.

Ufuatiliaji wa rasilima za Umma ‘PETS’ ni ule mpango ama utaratibu wa kwa kundi la watu, mtu mmoja mmoja au taasisi yoyote kufanya ufuatiliaji.

Ufuatiliaji wa rasilimali za umma, hauna maana kuwa, kwa mfuatiliaji anaingilia majukumu ya serikali au mfadhili anaejenga jengo la umma mfano skuli au hospitali.

Kazi hii ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma, katika miaka kadhaa ilikuwa maarifu zaidi Tanzania bara, kwa kule wananchi kuhoji, kuuliza na kutaka ufafanuzi wa matumizi ya fedha za umma.

Wananchi kadhaa wa Tanzania bara kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa, walizoeshwa kuwa na mikutano ya kujadili bajeti za utekelezaji kuanzia ngazi ya kata.

Ambapo hapo walikuwa na nguvu za ufuatiliaji wa fedha za umma, zinavyotumika na wakati mwengine hadi wananchi kuikataa miradi.

Pengine waligundua kuwa, gharama za ujenzi na thamani ya miradi husika, mfano ujenzi wa vituo vya afya hauendani.

UZEOFU WA ZANZIBAR
Zanzibar suala hili wala halikua maarufu masikioni na machoni mwa wananchi, na hata viongozi wenyewe, wakidhani kuwa fedha za umma, hakukua na mtu mwenye ubavu wa kufuatilia.

Ingawa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 23 kimeweka bayana, haki na uhuru wa wananchi kusimamia ufuatiliaji wa rasilima za umma.

Ambapo kifungu hicho cha 23 (3) kimesema ‘watu wote watatakiwa na sheria kulinda vizuri mali ya Zanzibar na kwa pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa Zanzibar kwa makini.

Hapa tunajifunza kuwa, suala la ufuatiliaji wa rasilima za umma kwa Zanzibar, kumbe lipo kikatiba, na ndio maana hata Baraza letu la Wawakilishi, limeanzisha sheria ya Manunuzi kwa lengo la kulinda fedha za umma.

PACSO INAFANYAJE?
Mwenvuli wa Asasi za Kiraia kisiwani Pemba ‘PACSO’ ni moja ya asasi iliyokusanya zaidi ya asasi 50 za Pemba, wakiwa na malengo kadhaa.

Moja ya majukumu yake, ni kuhakikisha wanachama wao ambao ni asasi moja moja, kuwa na uwezo wa kujisimamia wenyewe, badala ya kutegemea wafadhili moja kwa moja.

Katibu Mkuu wa ‘PACSO’ Sifuli Ali Haji, anasema walianzisha PACSO tokea mwaka 2005, na tayari wameshapata miradi kadhaa.

Mmoja wa miradi anasema ni ule wa mwaka 2016, ambao ulikuwa unalenga kufanya ufuatiliaji wa rasilimi za umma, ambapo hapo, waliangalia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha kifusi.

Mradi huo ulihusisha baadhi ya barabara zilizomo wilaya ya Wete na Micheweni kwa wakati huo, ambapo waliupata baada ya kuuomba kwa wafadhili wao the foundation for Civil Society ya Tanzania bara.

PACSO, ilifanikiwa tena kuutia mikononi mradi mwengine wa ufuatiliaji wa rasilima za umma, safari hii ukitekelezwa kwa mkoa wa kusini Pemba.

Mradi huu kwa mujibu wa Mwenyekiti wa bodi ya PACSO Ali Mohamed Shela, anasema uliangalia ufuatiliaji wa rasilimali za umma kwenye ujenzi wa skuli.

“Ule mradi kama huu ule wa mwaka 2016, uliangalia ujenzi wa matumizi ya fedha kwa barabara za kiwango cha kifusi za Mkoa wa kaskazini Pemba, lakini huu umetekelezwa Mkoa wa kusini Pemba,’’anasema.

Mwenyekiti huyo wa Bodi, alisema kiasi cha shilingi milioni 34, zilitumika katika ujenzi wa skuli hizo, ambapo wao waliangalia suala la ushirikishwaji wa wananchi.

Jambo jengine ambalo waliliangalia, ni iwapo fedha hizo zilitumika vyema, na hasa suala la wananchi kuanza kushirikisha kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Mratibu wa mradi huu Mohamed Najim Omar, anasema baada ya uzinduzi, kilichofuata ni kuzijengea uwezo kamati za skuli, shehia na maafisa wengine.

Anasema, lengo hasa ilikuwa ni kuwapa elimu wanakamati hizo za skuli za Madungu na Chambani, ili kisha waweze kuhoji, kufuatilia na kuuliza juu ya matumizi ya rasilima za umma.

Anasema, mradi huo waliugawa kwa awamu mbili, ambapo ya kwanza ilikuwa ni kuutambulisha mradi na kufanya mafunzo kwa wadau husika, ambapo zaidi ya washiriki 50 walishiriki.

“Ndani ya hao, 50 wapo wenye ulemavu, waandishi wa habari, watendaji wa baraza la mji Chake chake, watendaji wa wizara ya Elimu, Wizara ya fedha, ZAECA pamoja na baadhi ya watendaji wa PACSO,’’anasema.

Mratibu, anasema baada ya kumalizika kwa shughuli kadhaa ndani ya awamu ya kwanza, kisha awamu ya pili iling’oa nanga kwa kasi kubwa.

Ambapo, sasa zile kamati ambazo zilishapewa mafunzo ya ufuatiliaji kwenye awamu kwanza ya mradi, sasa zilijengewa uwezo ili kuandaa ripoti.

Anasema mradi ulitaka kuona moja kwa moja, namna ambavyo rasilimali za umma zimetumika kwenye mirdi ya ujenzi kwa skuli za msingi za Madungu na ile ya sekondari ya Chambani.

“Mradi ulielekeza nguvu ya utekelezaji wizara ya Elimu tena ni kwenye skuli ya Madungu wilaya ya Chake chake na ile ya sekondari ya Chambani wilaya ya Mkoani mkoa wa kusini Pemba,’’anafafanua.

Katibu mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, anasema kamati hiyo ambayo iliundwa na wajumbe 20 kutoka taasisi za ZAECA, Wizara ya fedha, baraza la mji Chake chake, waandishi wa habari, kundi la wenye ulemavu pamoja na wahandisi wa kujitegemea.

Kisha kamati hii ilipewa mbinu ya kutengeneza madodoso maalum, ambapo kazi hii iliongozwa na mtaalamu kutoka Afisi ya mtakwimu mkuu wa serikali kisiwani Pemba.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mwenyekiti wa bodi ya ‘PACSO’ Ali Mohamed Shela, alisema anatarajia kamati hiyo iibuke na matokeo ya mradi kama ilivyo lengo la asasi yao.

“Mafunzo haya ni makusudio maalum kwa kamati hii, ambayo inakwenda kwa jamii kukusanya taarifa za ujenzi wa majengo ya skuli, na kisha kutueleza ikiwa rasilimali za umma zimefanywa kisheria,’’anasema.

Ingawa Mratibu wa mradi Mohamed Najim Omar, anasema baada ya Kamati hiyo kukusanya taarifa wakiongozwa na madodoso hayo, kisha walikabidhiwa ripoti.

“Tayari ripoti hiyo kabla ya kuiwasilisha kwa wafadhili, kwanza iliwasilishwa mbele ya wadau na kutoa changamoto na hoja zao mbali mbali, ambazo zililenga kuimarisha ripoti hiyo,’’anasema.

Mratibu anasema, lengo la kuiwasilisha kwa wadau ripoti hiyo, ni kujiridhisha kwa vile walikuwa nao bega kwa bega, tokea kuanza kwa mradi huo mwezi Julai mwaka 2019.

MATOKEO YA MRADI
Moja kati ya jambo kubwa, ambalo ‘PACSO’ wanasema wanajivunia ni jamii kupata hamasa ya kufanya ufuatiliaji wa rasilimali za umma, jambo ambalo hapo kabla halikuwepo.

Jengine ambalo wanasema ni kama matunda ya mradi ni kuharakisha ujenzi wa skuli hizo, ambao awali kabla ya mradi ulianza kwa kusua sua.

Mratibu huyo anasema, hata kule kukubaliwa na wizara ya Elimu na baraza la mji wa Chake chake, kuutekeleza mradi huo ndani taasisi zao, sio jambo dogo.

“Unajua kuwa, mradi huu kama vile unafuatilia matumizi ya fedha za serikali, sasa maafisa wa taasisi hizi kukubali kuutekeleza, ni matokea pia ya mradi,’’anasema.

Hata Katibu mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, anasema jengine ambalo wanajivunia baada ya kumalizika kwa mradi huo, ni wananchi kuwa na muamko wa ufuatiliaji.

Aidha Sifuni anasema, matokeo mengine ambayo ni makubwa ni kufanikiwa kutekeleza mradi na kumalizika kwa wakati, kwani sasa wameshaituma ripoti kwa wafadhili.

WADAU WA MRADI WANASEMAJE
Kassim Ali Omar ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ufuatiliaj wa rasilimali za umma ‘PETS’ ambayo iliasisiwa na mradi huo ulioendeshwa na PACSO, anasema mradi huo ni wa aina yake.

Anasema mradi huo kwa upande wao, baada ya kukusanya taarifa na kuandika ripoti waligundua ushirikishwaji wa mdogo wa kamati husika.

“Lakini pia hakuna utamaduni mzuri wa wanakamati za skuli na zile kamati za maendeleo, kuhudhuria kwenye vikao, jambo linalopelekea kukosa taarifa mtiririko,’’anasema.

Lakini mjumbe wa kamati hiyo Robart Migua Ndalami, anasema kamati hiyo iligundua kuwa, bado baadhi ya taratibu hazifuatwi za matumizi ya fedha za umma.

“Upo utaratibu ambao una dalili za harufu ya rushwa, maana wananchi na hasa wanakamati, hawafahamu namna ya kupokea bajeti na matumizi yake,’’anasema.

Mjumbe Suleiman Mansour kutoka kundi la watu wenye ulemavu, alisema lazima sasa kazi zote za ujenzi kwa majengo ya umma, zabuni zake ziwe wazi.

Anasema, yapo majengo yamekuwa yakikosa zabuni za hadhari na kisha fedha zake wananchi na kamati husika kukosa kuzifuatilia kwa karibu.

Afisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salum, alisema mradi huo ni mzuri ingawa kwao wamekuwa wakifuata maagizo yote ya manunuzi na ujenzi.

“Wakati mwengine taarifa za ujenzi na matumizi hukumbwa na utoro wa wanakamati, hivyo inawezekana waliohojiwa ikawa ni wale watoro, lakini wizara inajitahidi kutoa taarifa,’’anasema.

Anasema, wamekuwa wakipokea maombi ya ujenzi wa majengo ya skuli, hivyo anaamini suala la kushirikishwa bila shaka huanzia hapo.

Mtendaji wa Baraza la Mji Chake chake Khatib Bakar, amesema mradi ulioandeshwa na PACSO, umewaamsha watendaji wao, hasa katika kuzingatia matumizi sahihi ya fedha.

Alisema ingawa zipo taratibu za manunuzi na ujenzi, lakini mradi huo umewapa nguvu, kuona sasa taratibu zilizopo zinafuatwa kikamilifu.

Sheha wa shehia ya Chambani wilaya ya Mkoani, Omar Abdalla anasema mradi huo wa ufuatiliaji wa rasilimali za umma ni mzuri, na umewapa mwamko wa kufuatilia.

Anasema, sasa mradi wowote utakaochomoza ndani ya shehia yake, anaweza kujua kuhoji na kuuliza namna ambavyo utatekelezwa.

“Mradi ulioaendeshwa na PACSO wa ufuatiliaji wa rasilimali za umma ‘PETS’ ambao ulifanyakazi ndani ya shehia yangu, umetuamsha na kutupa uthubutu kwa sasa,’’anasema.

Asha Mohamed Omar wa Madungu wilaya ya Chake chake, anasema mradi huo ni mzuri maana umewagusa moja kwa moja.

Mwalimu mkuu skuli ya sekondari Chambani, Sinani Zubeir Faki, anasema kwa sasa, ujenzi wa madarasa umeshakamilika kwenye skuli yake, na mradi wa ‘PETS’ ulikuwa chachu.

“Pengine leo hii kama mradi wa ufuatiliaji wa rasilimali za umma ‘PETS’ haukupita kwenye skuli yangu, huwenda twengezorota na kuchelewa kuhamia,’’alieleza.

MAPENDEKEZO KUTOKA PACSO
Fedha za ujenzi wa majengo ya umma, lazima ziwe wazi, kuanzia siku ya kwanza ya kutangaaza zabuni pamoja na ufunguzi wake.

Jengine ambalo Mratibu wa mradi huu Mohamed Najim Omar anapendekeza, wananchi wapewe furasa ya kuchagua miradi waitakayo na kushirikishwa.

Katibu mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji anasema, kumbu kumbu za ujenzi na matumizi ziwepo katika kila eneo, mfano skuli na wizara husika.

Anapendekeza pia, kuwepo kwa mfumo ambao wananchi wanaweza kuhoji na kuuliza jinsi ya mradi unavyotekelezwa na kujua bajeti hiyo inatoka wapi.

Wiki iliyopita, kwenye mkutano wa tathmini uliofanyika Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi, Katibu Mkuu wa PACSO Sifuni Ali Haji, alizitaka NGOs kuacha woga.

“Mradi kama huu, wapo wengine tumekuwa tukiwaalika, lakini hawahudhurii kwa woga, wakati kasi ya serikali ya awamu ya nane ilivyo, nasi tumekwenda sambamba,’’anasema.